Friday, December 7, 2012

TAIFA STARS: ANGUKO KUU KAMPALA



TANZANIA imepoteza nafasi ya kucheza fainali ya Kombe la Chalenji baada ya Kilimanjaro Stars na Zanzibar Heroes kufungwa na Uganda na Kenya kwenye michezo ya nusu fainali iliyofanyika jana kwenye Uwanja wa Namboole, Kampala.

Katika mechi hizo, Kili Stars waliondolewa na wenyeji Uganda kwa kichapo cha mabao 3-0, huku ndugu zao Heroes waliondolewa kwa changamoto ya mikwaju ya penalti 4-2 na Kenya baada ya dakika 120 kumalizika kwa sare ya bao 2-2.
Uganda walianza kwa kasi na dakika ya sita, Robert Ssentongo alipiga shuti kali lililodakwa kwa ustadi na kipa Juma Kaseja, kabla ya Emmanuel Okwi kuwafungia wenyeji bao la kuongoza dakika 11 kwa shuti kali baada ya kupokea pasi ndefu ya Moses Oloya.

Stars waliamka na kuanzisha mashambulizi na dakika 19, mpira wa kichwa wa Erasto Nyoni uligonga besela kabla ya kuokolewa na mabeki wa Uganda.

Uganda walilazimika kufanya mabadiliko mapema baada ya Okwi kutolewa kufuatia kuumia na nafasi yake kuchukuliwa na Hamis Kiiza.

Kiiza alipokea pasi ndefu kutoka upande wa kushoto na kuingia kwa kasi ndani ya eneo la hatari na kupiga krosi iliyounganishwa kwa umakini na Ssentongo dakika 52 na kumaliza ndoto ya Tanzania kusonga mbele.

Ssentongo alifungia Uganda bao la tatu akimalizia mpira uliotemwa na kipa Kaseja dakika 73, lakini dakika 84 taa za uwanja wa Namboole zilizimika na kusababisha mchezo kusimama.

Awali, Zanzibar Heroes mara mbili walipata mabao ya kuongoza, lakini walishindwa kulinda uongozu huo na kujikuta wakilazimishwa sare 2-2 kabla ya kuondolewa kwa mikwaju ya penalti 2-4.

Baada ya sare hiyo, changamoto ya mikwaju ya penalti ilichukua nafasi yake, ambako Heroes ilipata mbili zilizofungwa na Aggrey Morris na Samih Nuhu, huku Khamis Mcha na Issa Othaman wakikosa, wakati Kenya walipata penalti zote nne zilizopigwa na Mike Baraza, Joakins Atudo, Edwin Lavatsa na Abdallah Juma.

Awali, nyota wa Azam, Mcha aliifungia Heroes bao la kwanza dakika 21 akiunganisha vizuri krosi ya Amir Hamad, hata hivyo bao hilo lilidumu kwa dakika nane, kabla ya Kenya kusawazisha baada ya nahodha wa Zanzibar, Nadir Haroub kujifunga wakati akijaribu kukoa mpira mrefu wa juu na kumpita kipa wake Mwadin Ally.

Beki Morris alifungia Heroes bao la pili kwa mkwaju wa penalti dakika 75, baada ya beki wa Kenya, Joakins Atudo kumwangusha ndani ya eneo la hatari Juma Jaku. Hata hivyo, bao hilo lilidumu kwa dakika tano kabla ya Baraza kusawazisha kwa Kenga akiunganisha kwa kichwa kona ya Paul Wene

No comments:

Post a Comment

AddThis

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...