KABWE ZUBERI ZITTO: MABILIONI YA USWISI – TUSIGEUZWE MAZEZETA
Jumanne tarehe 20
Novemba 2012, baadhi ya vyombo vya habari vimebeba habari zinazohusu matamshi
ya Waziri wa Utawala Bora ndugu George Mkuchika kuhusu sakata ya mabilioni ya
Uswisi.
Waziri amesema kwamba
Serikali ya Uswisi inataka majina ya Watanzania walioficha fedha huko ndio
waweze kusaidia uchunguzi. Habari kama Hiyo, yenye maudhui na malengo hayo hayo
iliandikwa na Gazeti la The Guardian on Sunday la tarehe 18 Novemba 2012.
Nimeona ni vema nitoe
kauli yangu rasmi kuhusu suala hili. Lengo ni kuweka rekodi sawa juu ya Azimio
la Bunge na kwamba Serikali inapaswa kutekeleza Azimio na sio kutoa kauli tata
za kukata tamaa.
Moja, Suala hili japo
sio jipya lakini limeandikwa kama ni jambo jipya. Suala la Serikali ya Uswisi
kutaka majina lilisemwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali wakati akichangia hoja
binafsi niliyowasilisha Bungeni na pia wakati akileta maombi yake ya kuiondoa
hoja ambayo yalikataliwa na Bunge.
Kama sio sababu mpya
ni kwanini imeibuka upya na kwa kasi? Ni wazi Serikali inajihami kwa kuona kuwa
itashindwa kutekeleza azimio la Bunge. Watanzania wasikubali propaganda hii ya
Serikali.
Bunge limeagiza
Serikali kufanya uchunguzi kwa kutumia njia za kiserikali au wachunguzi binafsi
wa kimataifa. Kwa nini Serikali inaanza kubwabwaja ilhali wala haijaanza kazi
hiyo? Serikali inajaribu kuficha nini?
Kwa nini baada ya wiki iliyopita Benki
Kuu kufanya uchunguzi kwenye Mabenki ya Biashara jijini Dar es Salaam na namna
fedha zimekuwa zikipelekwa nje (international transfers), leo Serikali inakuja
na kauli za kukakata tamaa? Kunani?
Pili, Watanzania
wajue kwamba Taifa la Swiss limejengwa na linajengwa kwa fedha hizi za wizi
ambazo watu mbalimbali duniani wanaiba au kukwepa kodi kwenye nchi zao na
kuzificha huko. Serikali ya Swiss hata siku moja haiwezi kutoa ushirikiano kwa
Serikali ya Tanzania katika suala kama hili. Ndio maana Azimio la Bunge
linataka wachunguzi binafsi ambao hawatahitaji ushirikiano wa Serikali ya
Swiss.
Nawakumbusha kwamba mwaka 1997 mara baada ya
Joseph Desire Mobutu kuangushwa na Rais Joseph Kabila kule Kongo – Kinshasa,
Serikali ya Swiss iliitaka Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo
kuonyesha ushahidi kuwa hela hizo za Mobutu zilikuwa zimepatikana kwa njia
haramu! Waswiss walitaka Kabila awakakikishie kuwa fedha zile zaidi ya dola
bilioni nane za Kimarekani Mobutu hakuzipata kihalali ndio waweze kuzirejesha.
Zaire ilikadiriwa
kuwa na zaidi ya dola za Kimarekani bilioni thelathini katika Mabenki ya nje ya
nchi hiyo. Majibu ya aina aina hii ni majibu ‘standard’ ambayo kila nchi
inapewa. Hata Marekani ilipokuwa inafuatilia wakwepa kodi wao walijibiwa hivi
hivi.
Hatimaye Serikali ya Marekani ikaamua kununua taarifa hizo na kuwakamata
wakwepaji kodi wao walioficha fedha Uswisi. Hao ndio Waswiss ambao Serikali ya
Tanzania inashabikia majibu yao.
Bila
Aibu Mawaziri wetu wanayanukuu majibu ya Waswiss kama kasuku. Tunasahau
historia haraka sana. Tunakuwa kama mazezeta.
Tusiwe
Taifa la mazezeta. Mabwege na mazezeta huimba kila wanachoambiwa kuimba. Sasa
Serikali ya Tanzania imekuwa msemaji wa Serikali ya Swiss badala ya kuchunguza
utoroshaji wa fedha haramu na kisha kutoa taarifa Bungeni.
Naitaka Serikali
ianze uchunguzi mara moja kama namna ilivyoelekezwa na Bunge. Suala hili sio
suala la kisiasa, sasa ni Azimio la Bunge ambalo linahitaji kutekelezwa
kikamilifu. Suala hili sio suala la Zitto Kabwe tena, ni suala la Bunge, ni
suala la Wananchi. Wananchi hawataki uzezeta wa watu waliopewa dhamana ya
kutekeleza Azimio lao.
Kama hawawezi wapishe
watu wenye uwezo wa kusimamia maslahi ya Watanzania kwa kuchukua hatua stahili
za kuchunguza utoroshaji mkubwa wa fedha za kigeni, ukwepaji mkubwa wa kodi na
ufisadi uliopelekea Watanzania kuficha mabilioni kwenye mabenki nje ya
Tanzania.
Hatutakaa kimya mpaka
tuone mwisho kamilifu wa suala hili. Utekelezaji wa Azimio la Bunge itakuwa ni
salamu tosha mafisadi na watoroshaji wa fedha haramu kwamba hawana pa kujificha
na Tanzania sio Taifa la kuchezeachezea.
Lazima tushinde vita hii. Anayeona hawezi
kutuongoza kuishinda atupishe mapema. Hatupaswi kuwa Taifa la Mazezeta.
Watanzania sio mabwege tena, Mwakyembe alipata kusema.
Kabwe Zuberi Zitto, Mb Kigoma Kaskazini.
No comments:
Post a Comment