Monday, October 1, 2012





          TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete anaanza Ziara ya Kikazi ya Marekani na Ziara Rasmi ya Kiserikali ya Canada akianzia mjini New York, Marekani leo, Jumatatu, Oktoba Mosi, 2012.

Rais Kikwete na ujumbe wake uliondoka nchini usiku wa jana, Jumapili, Septemba 30, 2012, na utawasili mjini New York, Marekani mchana wa leo tayari kwa ziara hiyo ya Marekani. Rais Kikwete atakuwa Marekani kwa siku mbili kabla ya kwenda Canada kwa ziara Rasmi ya Kiserikali ya siku mbili.

Katika ziara yake mjini New York, Marekani, Rais Kikwete atakutana na kufanya mazungumzo na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Mheshimiwa Ban Ki Moon ofisini kwa Katibu Mkuu huyo kesho asubuhi Oktoba 2, 2012.

Baada ya mazungumzo hayo, Rais Kikwete ataungana na Mheshimiwa Ban Ki Moon, Meya wa Jiji la New York na Mfadhili Mkubwa wa Misaada ya Kibinadamu Duniani, Mheshimiwa Michael Bloomberg; Mama Helen Agerup ambaye ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Misaada ya Kibinadamu ya H&B Agerup na Dkt. Kelly J. Henning, Mkurugenzi wa Mipango ya Sekta ya Afya ya Taasisi ya Bloomberg Philanthropies kwenye Uzinduzi wa Matokeo ya Mpango ya Ubunifu wa Afya ya Akinamama katika Tanzania.

Kwenye sherehe hiyo iliyopangwa kufanyika kwenye ukumbi uitwao Green Room kwenye makao makuu wa Umoja wa Mataifa, Rais Kikwete, Mheshimiwa Ban Ki Moon, Meya Bloomberg na mama Helen Agerup kwa pamoja watazindua Matokeo ya Mpango huu uitwao Innovative Maternal Health Program.

Kwenye shughuli hiyo pia Meya Bloomberg atatangaza matokeo ya miaka mitatu ya misaada ya kiafya chini ya mpango huo kwa akinamama iliyotolewa na taasisi ya inayomilikiwa na Meya Bloomberg ya Bloomberg Philanthropies.

Aidha, kwenye shughuli hiyo, Meya Bloomberg atatangaza misaada mpya wa mabilioni ya fedha kuboresha afya ya akinamama katika Tanzania chini ya mpango huo na atatangaza mshirika mpya ambaye atasaidiana na taasisi ya Bloomberg Philanthropies katika kuunga mkono huduma bora za afya kwa akinamama wa Tanzania.

Katika Tanzania, misaada ya taasisi ya Bloomberg Philanthropies huelekezwa katika maeneo ya vijijini yasiyokuwa na huduma bora zaidi kwa kiafya na huduma ambazo hutolewa ni zile za kuokoa maisha ya akina mama hasa wakati wa uzazi.

Tokea mwaka 2006, taasisi hiyo imetoa kiasi cha dola za Marekani milioni 11.5 Fedha hizo ni sehemu ya kiasi cha dola za Marekani milioni 330 ambazo zilitolewa na taasisi hiyo kwa nchi mbali mbali duniani kwa mwaka jana peke yake.

Taasisi hiyo hufanya kazi ya kuendeleza maeneo matano duniani ambayo ni Usanii, Elimu, Mazingira, Ubunifu katika Serikali na Afya ya Umma.

Rais Kikwete ataondoka Marekani kwenda Canada keshokutwa Jumatano Oktoba 3, 2012 kwa ajili ya Ziara Rasmi ya Kiserikali ya siku mbili katika nchi hiyo kwa mwaliko wa Gavana Jenerali wa nchi hiyo, Mheshimiwa David Johnston.

Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
Dar es Salaam.
1 Oktoba, 2012



 



EWURA: YASHINDA KESI  DHIDI YA MAKAMPUNI YA MAFUTA.

KESI iliyofunguliwa na kampuni 13 zinazouza mafuta, ikiwamo BP Tanzania Limited dhidi ya Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), imetupiliwa mbali baada ya kushindwa kuthibitisha hasara waliyopata kwa bei za mafuta kushuka.

Kesi hiyo ilitupiliwa mbali mwishoni mwa wiki na Baraza la Rufaa la Ushindani, mbele ya jopo linaloongozwa na Mwenyekiti, Jaji Razia Sheikh. Wajumbe waliokuwa katika jopo hilo ni pamoja na Dk. M. Bundara na Ali Juma.

“Kutokana na mazingira yaliyokuwapo, mdaiwa (EWURA), alifuata sheria katika kutangaza bei mpya ya mafuta, lakini walalamikaji walikaidi kukubaliana na uamuzi huo.

“Kwa hiyo, malalamiko yao hayana msingi na jopo linayatupilia mbali na walalamikaji wanatakiwa kuilipa EWURA gharama za kesi,” alisema Jaji Sheikh.

Jaji Sheikh akisoma uamuzi huo, alisema EWURA kwa mamlaka waliyonayo walitangaza bei mpya ya mafuta ambayo ilitakiwa kuanza kutumika Agosti 3, mwaka jana kwa kuzitaka kampuni za mafuta kuuza mafuta kwa gharama yoyote lakini isizidi kiasi kilichopangwa.

Alisema kuwa, EWURA wakati ikishusha gharama za mafuta, ilizingatia vigezo vyote kisheria na maslahi ya wanunuzi, wawekezaji wa mafuta pamoja na Serikali.

“Hakuna ushahidi wa kuonyesha kwamba EWURA wakati wanapunguza bei ya mafuta hawakuzingatia maslahi ya wawekezaji, wanunuzi na uchumi wa nchi kwa ujumla.

“Wakata rufaa wameshindwa kuleta ushahidi wa kuonyesha athari walizopata kutokana na bei mpya, upo ushahidi miongoni mwao waliendelea kufanya biashara na kusambaza mafuta,” alisema.

Kampuni zilizofungua kesi dhidi ya EWURA kwa kushusha bei ya mafuta Agosti mwaka jana ni BP Tanzania Limited, Engen Petroleum Tanzania Limited, Camel Oil, Oilcom, Total, Gapco, Hass Petroleum, Oryx, MGS, Lake Oil, Moil na Acer Petroleum Tanzania Limited.

Katika shauri hilo, walalamikaji hao waliwasilisha madai 10 wakidai kwamba, wakati wanashusha bei ya mafuta, EWURA walishindwa kuzingatia gharama za kusambaza mafuta nchini, hawakujali maslahi yao, walishindwa kutoa uwiano kati ya wanunuzi, wasambazaji na kwamba mamlaka hiyo iliwataka walalamikaji kuuza mafuta kwa hasara.

Jaji Sheikh alisema kuwa, EWURA hawakuwalazimisha wasambazaji wa mafuta kuuza kwa bei moja bali waliwaruhusu kuuza kwa gharama yoyote ya chini kwa ajili ya ushindani wa kibiashara lakini wasizidi bei halisi iliyotangazwa ambapo faida ilizingatiwa.

Jaji huyo alisema kwamba, walalamikaji walileta mashahidi watatu lakini hakuna ushahidi wa kuthibitisha kwamba, kila mlalamikaji alipata hasara kiasi gani baada ya gharama za mafuta kushuka.

Agosti mwaka jana, kampuni zinazouza mafuta zilitishia kugoma kuuza mafuta wakipinga agizo la Serikali la kuwataka kuuza nishati hiyo kwa bei isiyozidi Sh 2,004 kwa lita kwa madai kwamba watapata hasara ukilinganisha na gharama wanazotumia.

Hata hivyo, EWURA ilifafanua kwamba, atakayeendelea kuuza mafuta kwa bei ya juu tofauti na iliyopangwa, atatozwa faini ya Sh milioni 3 na Sh milioni moja kila siku hadi atakapojirekebisha.

“Kulingana na kiasi cha tozo iliyopunguzwa kutoka kwa mamlaka na taasisi za umma, sasa wafanyabiashara wa mafuta watakuwa wanapata faida ya Sh 110 kwa kila lita, kabla ya mgogoro huo wafanyabiashara hao walikuwa wakipata faida ya Sh108 kwa lita,” ilisema taarifa ya EWURA.

Wakati wa shauri hili walalamikaji waliwakilishwa na Wakili, Fatuma Karume akisaidiana na Madina Chenge na EWURA iliwakilishwa na Wakili Galeba pamoja na Kabakama.

No comments:

Post a Comment

AddThis

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...