Monday, October 29, 2012

JK WANAOCHOCHEA UKABILA NDO WANAOCHOCHEA UDINI LEO 

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete jana, Jumapili, Oktoba 28, 2012, ameanza ziara ya siku nne kukagua shughuli na kuzindua miradi ya maendeleo katika Mkoa wa Kilimanjaro kwa kuwaambia Watanzania kuwa moto wa dini ambao umeanza kujitokeza katika Tanzania hautakuwa na mshindi.

Rais Kikwete ameanzia ziara yake kwenye Wilaya ya Same ambako amehutubia mkutano wahadhara kwenye eneo la Stendi ya Mabasi ya mjini Same ambapo amewaambia mamia ya wananchi kuwa baada ya watu wasioitakia Tanzania mema kushindwa 
kuwafarakanisha Watanzania kwa kutumia ukabila sasa wamegeukia dini.

“Kuna watu hawana raha na utulivu na amani ya nchi yetu. Walijaribu kutufarakanisha kwa kutumia ukabila lakini hili lilishindikana na sasa wamegeukia dini. Lakinindugu zangu moto wa dini hautakuwa na wa kuuzima na hautakuwa na mshindi,” Rais Kikwete amewaambia wananchi kwenye mkutano huo.

Amewataka Watanzania kuendelea na utulivu wao wa kidini na wakatae kufarakanishwa kwa tofauti za dini.

“Ndugu zangu, siku zote tumekuwa na dini zetu, kila mmoja akiwa na uhuru wake wa kuabudu anachokitaka na kukiamini na kwa namna anavyotaka yeye. Ni muhimu tuendelee kuheshimu tofauti zetu za dini bila kuzigeuza tofauti hizokuwa chimbuko na sababu ya ugomvi.”

Rais Kikwete pia amewahakikishia wananchi wa Same kuwa Serikali imedhamiria kumaliza tatizo la maji katika maeneo ya wilaya hiyo na wilaya za jirani za Mwanga na Korogwe katika Mkoa wa Tanga.

Amesema kuwa mradi mkubwa wa kusambaza maji katika vijiji 34 katika wilaya hizo kutoka Bwawa la Nyumba ya Mungu utaanza kutekelezwa Februari mwakani.

 Mradi huo wenye thamani za dola za Marekani bilioni 34 utawahudumia wananchi katika vijiji 14vya Wilaya ya Same na utachukua kiasi cha miezi 18 kukamilika.

Rais Kikwete ataendelea na ziara yake leo, Jumatatu, Oktoba 29, 2012 kwa kuzindua Kiwanda cha Tangawizi kilichoko Mamba Miamba na kufanya mkutano hadhara na wananchi.
 Baadaye kesho, Rais Kikwete atazindua Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Asha-Rose Migiro iliyoko Mwanga.

Imetolewa na:
Kurugenziya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu. Dares Salaam.
29Oktoba, 2012

No comments:

Post a Comment

AddThis

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...