Wednesday, October 10, 2012



MAELEZO YA WAZIRI WA AFYA NA USTAWI WA JAMII MHE. DKT HUSSEIN A.  MWINYI KWA  WAANDISHI WA HABARI KUHUSU DAWA BANDIA YA KUPUNGUZA MAKALI YA UKIMWI YENYE JINA LA BIASHARA TT-VIR 30 TOLEO NAMBA 0C.01.85

Picture
WAZIRI WA AFYA NA USTAWI WA JAMIII DK .HUSSEIN MWINYI

1.0          UTANGULIZI
Mnamo mwanzoni mwa mwezi Agosti 2012 Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kupitia Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) kwa kuzingatia Sheria ya Chakula, Dawa na Vipodozi sura  219 ilibaini kuwepo kwa dawa bandia ya kupunguza makali ya UKIMWI aina ya TT–VIR 30  zenye toleo Na. 0C.01.85  katika hospitali ya wilaya ya Tarime.

Baada ya kubaini tatizo hili, Wizara kupitia TFDA ilichukua hatua zifuatazo;-

                      i.        Ilifanya ukaguzi kwenye vituo vya kutolea huduma za afya katika Mkoa wa Mara na baadaye ukaguzi wa kina katika mikoa mingine nchi nzima kwa kushirikiana na vyombo vya usalama. Ukaguzi huu ulifanyika kati ya tarehe 6-31 Agosti, 2012.  Ukaguzi pia ulihusisha Bohari ya Dawa (MSD) Makao Makuu na Kanda pamoja na Kiwanda cha Tanzania Pharmacentical Industries Limited ambacho ndicho kilitengeneza dawa hiyo na kuchukua sampuli za dawa husika kwa ajili ya uchunguzi wa kimaabara.

                     ii.        Kuwataarifu Waganga Wakuu wa Mikoa yote nchini na kuwaelekeza wasimamishe matumizi ya dawa toleo namba 0C.01.85 katika vituo vyote vya kutolea huduma za afya katika mikoa yao. Aidha, walielekezwa kuiondoa dawa hiyo kwenye vituo vya kutolea huduma za afya na kuirudisha kwa msambazaji ambaye ni Bohari ya Dawa (MSD).

                    iii.        Kufanya uchunguzi wa kimaabara ili kuainisha viambata vya dawa hiyo.

2.0          MATOKEO YA UKAGUZI NA UFUATILIAJI

Kufuatia ukaguzi na ufuatiliaji huo, pamoja na  uchunguzi wa kimaabara yafuatayo yamebainika:
a.     Dawa yenye jina la biashara TT-VIR 30 toleo namba 0C.01.85 ni bandia kwa mujibu wa Sheria ya Chakula, Dawa na Vipodozi Sura 219.

b.    Nyaraka zilizopo zinaonesha kuwa kiwanda cha “Tanzania Pharmacetical Industries Limited (TPI)” waliiuzia Bohari ya Dawa (MSD) dawa hiyo bandia toleo namba 0C.01.85.

c.     Dawa ya kupunguza makali mya UKIMWI ya TT-VIR30 yenye toleo Na. 0C.01.85 ilitengenezwa mwezi Machi, 2011 na kwisha muda wa matumizi mwezi Februari, 2013.



Makopo ya dawa za kupunguza makali ya Ukimwi yakitofautiana vifungashio. Kopo la kwanza kushoto linaonyesha dawa halisi ya kupunguza makali ya Ukimwi iliyokidhi viwango ikifuatiwa na makopo 3 yenye dawa bandia ya kupunguza makali ya Ukimwi yenye jina la biashara TT –VR 30 toleo namba 0c.01.85 yaliyotengenezwa na kiwanda cha Tanzania Pharmaceutical Industries Ltd. (Picha na Aron Msigwa – MAELEZO)

Picture
 d.    Dawa hiyo bandia, yenye toleo Na. 0C.01.85 ilikuwa na dawa zenye rangi mbili tofauti, njano na nyeupe.  Dawa zilizokuwa na rangi ya njano, zilikuwa na kiambata cha Efaverenz badala ya viambata aina ya Niverapine, Lamivudine na Stavudine vilivyopaswa kuwepo.  Vidonge vyenye rangi nyeupe vilikuwa na viambata vinavyotakiwa kuwepo yaani; Niverapine, Lamivudine na Stavudine kama ilivyokuwa kwenye labo.

e.     Vidonge vilivyokutwa kwenye vifungashio vya dawa husika, vilikuwa tofauti na vifungashio vilivyosajiliwa na TFDA (Caplet).

3.0          HATUA ZILIZOCHUKULIWA

a.     Matumizi ya dawa ya kupunguza makali ya UKIMWI aina ya  TT-VIR 30 toleo Na. 0C.01.85, inayotengenezwa na kiwanda cha TPI yamesimamishwa na dawa hiyo imeondolewa katika vituo vya kutolea huduma za afya na kurudishwa Bohari ya Dawa (MSD).
b.    Wizara kupitia TFDA, imesitisha uzalishaji wa dawa zote katika Kiwanda cha TPI Ltd hadi uchunguzi wa suala hili utakapokamilika.

c.     Wizara imesitisha usambazaji wa dawa zote zilizokwisha tengenezwa na kiwanda cha TPI ambazo ziko kwenye bohari za TPI hadi hapo uchunguzi wa suala hili utakapokamilika.

d.    Serikali imewasimamisha kazi Mkurugenzi Mkuu wa MSD, Mkuu wa Kitengo cha  Udhibiti Ubora (Quality Assurance Manager) pamoja na Afisa Uthibiti Ubora (Quality Assurance Officer).


e.     Wizara imehakikisha kuwa dawa za kupunguza makali ya UKIMWI zenye ubora unaotakiwa zinaendelea kupatikana katika vituo vya kutolea huduma za afya kote nchini.

f.     Waganga Wakuu wa Mikoa (RMOs) na Wilaya (DMOs) wamekumbushwa kuimarisha Kamati za Dawa na Tiba (Medicines and Therapeutic Committees) katika vituo vya huduma za afya, ambazo zina majukumu ya kusimamia upokeaji, uhakiki wa ubora na matumizi sahihi ya dawa na vifaa tiba.


4.         MATARAJIO
Wizara inaendelea kuimarisha mfumo na taratibu za uhakiki wa ubora, utunzaji usambazaji na matumizi ya dawa katika vituo vya kutolea huduma za afya kote nchini.


Mmmoja wa maafisa kutoka Mamlaka ya Chakula na Dawa Nchini (TFDA) ambaye hakutaka jina lake liandikwe kwenye vyombo vya habari akiwaonyesha waandishi wa habari Dawa badia za kupunguza makali ya Ukimwi (ARVS) zilizoondolewa katika vituo vya kutolea huduma mara baada ya kugundulika.

Picture 5.0        HITIMISHO

a.     Uchunguzi kupitia vyombo vya usalama unaendelea kuhusu suala hili kwa hatua zaidi za kisheria.

b.    Wizara itahakikisha kwamba kuna dawa za kutosha za kupunguza makali ya UKIMWI katika vituo vyote vya kutolea huduma za afya.

c.     Aidha  Wizara inatoa rai kwa jamii kutoa ushirikiano kwa kutoa taarifa pale wanapobaini kuwepo kwa dawa zwnye ubora wenye mashaka au uvunjivu wa Sheria inayosimamia ubora na usalama wa dawa

d.    Wizara inawahimiza wananchi waendelee kutumia dawa za kupunguza makali ya UKIMWI kwa kuwa dawa hiyo yenye mashaka imekwishaondolewa kwenye vituo vya kutolea huduma za afya.


No comments:

Post a Comment

AddThis

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...