Saturday, June 23, 2012

YANAYOTOKEA DUNIANI


 


                                                            MGOMO WA MADAKTARI TANZANIA  WASITISHWA

Mahakama kuu kitengo cha kazi nchini Tanzania imeamuru kusitishwa kwa mgomo wa madaktari uliopangwa kuanza leo kutokana na madhara makubwa yatakayotokana na mgomo huo.




Mahakama imetoa amri hiyo kufuatia madakatari kujiapiza kuanza mgomo usio na kikomo hii leo kufuatia kushindwa kufikia muafaka na serikali katika kuboresha maslahi yao.

Taarifa zaidi zinaeleza kuwa mgomo huo umesitishwa mpaka hapo madai ya serikali na Chama cha Madaktari Tanzania (MAT) yatakaposikilizwa na kutolewa uamuzi.

Amri hiyo ya Mahakama imetolewa kufuatia maombi namba 73 ya mwaka 2012 yaliyowasilishwa chini ya hati ya dharura na Mwanasheria Mkuu wa Serikali dhidi ya Chama cha Madaktari Tanzania (MAT) na kutaja sababu za msingi za kusitisha mgomo huo kuwa ni pamoja na madhara yasiyoweza kufidiwa kwa namna yoyote ile kama vile kupoteza maisha .

 

  MATOKEO YA UCHAGUZI WA URAIS NCHINI MISRI KUTOLEWA JUMAPILI

Tume ya uchaguzi ya Misri inasema kuwa itatangaza Jumapili matokeo ya uchaguzi wa duru ya pili ya uchaguzi wa rais uliofanywa mwisho wa juma lilopita.

Wafuasi wa Mohamed Mursi wakiandamana medani ya Tahrir

Kila mmoja kati ya wagombea hao wawili amedai kuwa ameshinda, na kwamba ataunda serikali ya kuleta umoja nchini.

Wafuasi wa Muslim Brotherhood wamekuwa wakiandamana katika medani ya Tahrir kati ya mji wa Cairo, kudai matokeo yatangazwe.




MAREKANI YAONYA KUTOKEA KWA MASHAMBULIO YA KIGAIDI NCHINI KENYA


Ubalozi wa Marekani nchini Kenya umeonya kwamba kuna tishio la shambulio la kigaidi kutokea mjini Mombasa karibuni, na umewataka watumishi wa serikali ya Marekani kuondoka katika mji huo.
Mji wa Mombasa, Kenya
Hii siyo mara ya kwanza kwa onyo kama hilo kutolewa.

Mwezi wa Oktoba mwaka jana, ubalozi wa Marekani ulisema kuna tishio la shambulio kwenye maeneo ambayo hutembelewa na wageni kama vile maeneo ya maduka mengi na vilabu vya starehe.

Wakati huo hakuna lilotokea, lakini hali katika nchi ya jirani, yaani Somalia, imezidisha wasiwasi.

Marekani imehusika na mapambano dhidi ya wapiganaji wa Kiislamu wa Somalia, ambao baadhi yao wana maingiliano na jamii kubwa ya Wasomali inayoishi Kenya.

Marekani haitaki kupita tena kwenye maafa ya mwaka wa 1998, ambapo ubalozi wake mjini Nairobi ulishambuliwa kwa mabomu, na watu zaidi ya 200 walikufa.

No comments:

Post a Comment

AddThis

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...