Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein akijibu maswali
ya waandishi wa habari jana alipokutana nao Ikulu mjini Zanzibar. Picha na
Martin Kabemba
Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein amesema hakuna
kiongozi yeyote wa Zanzibar mwenye mamlaka ya kuzungumzia msimamo wa Serikali
ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) kuhusu masuala ya Katiba na Muungano isipokuwa
yeye na kwamba kauli ambazo zimekuwa zikitolewa na Makamu wake wa Kwanza,
Maalim Seif Sharif Hamad ni zake binafsi au za chama chake.
Akizungumza na waandishi wa habari Ikulu, Zanzibar
jana juu ya tathmini ya uongozi wa Awamu ya Saba anayoiongoza, Dk Shein alisema
kuna changamoto kubwa za kuendesha Serikali ya Umoja wa Kitaifa na kwamba jambo
muhimu ni kuvumiliana.
Tangu kuanza kwa mchakato wa Katiba Mpya, msimamo wa
Maalim Seif ambaye pia ni Katibu Mkuu wa CUF, umekuwa ni kuundwa kwa Serikali
Tatu au ya Mkataba, ambao unapingana na ule wa CCM, wa kutaka Serikali mbili
kama ilivyo sasa.
Rasimu ya kwanza iliyotolewa na Tume ya Marekebisho ya
Sheria imependekeza kuwapo kwa Serikali Tatu, ya Muungano, Tanganyika na
Zanzibar.
“Serikali yangu haina msimamo wa jambo hilo. Kila
mwananchi ana uhuru wa kutoa maoni yake, ninaweza kutoa msimamo kutokana
yaliofikiwa na uamuzi wa chama changu na kila mtu anaweza kufanya hivyo na si
kuisemea Zanzibar na wananachi wake.”
Alimsifu Rais Jakaya Kikwete kwa dhamira yake ya
kusimamia suala la mabadiliko ya Katiba na mchakato ulivyokwenda na sasa taifa
linaelekea kupata Bunge la Katiba kabla ya kufanyika kwa kura ya maoni mwakani.
Akizungumzia Serikali ya Umoja wa Kitaifa, Dk Shein
alisema imefanikiwa kudumu kwa miaka mitatu sasa kutokana na kuvumiliana na
kufanya kazi kwa pamoja bila ya kutanguliza itikadi za kisiasa. “Nchi nyingi
zimejaribu hili zimeshindwa, lakini sisi tumefanikiwa kwa sababu tunavumiliana.
Hili linahitaji stahimili kubwa vinginevyo tutagawana mbao na sitaki hili
litokee kwenye uongozi wangu.”
Akizungumzia masuala ya Muungano, Dk Shein alisema
licha ya mchakato wa Katiba Mpya kuendelea, Serikali zote mbili (Muungano na
Zanzibar), zimeendelea kujadili masuala muhimu na changamoto zilizopo na kusema
siyo sahihi kubeza mgawo wa sasa wa mapato ya Muungano ambao Zanzibar inapata
asilimia 4.5.
“Jeshi la Wananchi na JKT (Jeshi la Kujenga Taifa)
wanatumia mabilioni mangapi, Mambo ya Nje, Mambo ya Ndani, Elimu ya Juu Sayansi
na Teknolojia... Sisi (Zanzibar tunatoa ngapi?)”
Uchumi
Akizungumzia ukuaji wa uchumi katika kipindi cha miaka
mitatu ya uongozi wake, Dk Shein alisema kumekuwa na ongezeko kubwa la
ukusanyaji wa mapato akisema katika mwaka wa fedha wa 2010/11 Sh181.4 bilioni
zilikusanywa na mwaka uliofuata wa 2011/12 makusanyo yaliongezeka hadi kufikia
Sh212 bilioni na mwaka wa fedha wa 2012/13 kiasi hicho kimeongezeka hadi
kufikia Sh266. 2 bilioni.
Alisema uchumi wa Zanzibar umekuwa ukiongezeka mwaka
hadi mwaka. Alisema mwaka 2010 uchumi ulikua kwa asilimia 6.4, mwaka 2011
asilimia 6.7, mwaka 2012 asilimia saba na mwaka huu unatarajiwa kukua hadi
kufikia asilimia 7.5.
No comments:
Post a Comment