Sunday, October 7, 2012



WAFANYAKAZI MGODI WA NORTH MARA MATATANI

WAFANYAKAZI zaidi ya 900 wa Mgodi wa Dhahabu wa North Mara Barrick (ABG) uliopo Nyamongo wilayani Tarime mkoani Mara wamelalamikia mambo mbalimbali yanayofanywa kwenye mgodi huo.

Katika malalamiko yao wafanyakazi hao wamesema hawaelewi nini itakuwa hatma ya ajira na mafao yao pale mgodi huo utakapouzwa kwa asilimia 74 za hisa kwa Kampuni ya Chines Gold.

Walitoa malalamiko yao mbele ya Naibu Waziri, Stephen Masele wa Nishati na Madini na Charles Kitwanga ambaye ni Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais, Mazingira walipotembelea na kuzindua miradi iliyotekelezwa na inayoendelea kujengwa na mgodi huo kwa gharama ya Shilingi bilioni 22.5 katika kipindi cha mwaka 2012 na 2015.

Ziara ya Naibu mawaziri hao ilifanyika katika mgodi huo Oktoba 5, mwaka huu ambapo wafanyakazi hao ambao baadhi yao ni wa kitengo cha kuendesha mitambo ya kusaga mawe mgodini hapo walitumia nafasi hiyo kuwasilisha malalamiko yao.

“Wafanyakazi wa Mgodi huu wa North Mara tunafanya kazi katika mazingira magumu, tunalipwa mishahara kidogo ukilinganisha na watu wanaotoka nje hata kama ujuzi wetu unazidi wa kwao pamoja na uzoefu.” “Hatuna uhakika na ajira zetu kwani kampuni hii inauza mgodi kwa Mchina, tunaomba tulipwe stahili zetu zote kulingana na muda tuliofanya kazi na kampuni hii ndipo tuanze Mkataba mpya na Mchina,” alisema William Magina.

Katika ziara hiyo Naibu mawaziri hao walitembelea na kuzindua miradi minane ikiwemo uzinduzi wa kisima cha maji kilichojengwa katika Shule ya Msingi Nyasangero, madarasa 12 ya kisasa na nyumba nane za walimu katika Shule ya Sekondari Ingwe na kukabidhi madawati 126 katika Shule za Msingi za Matare na Nyangoto.

No comments:

Post a Comment

AddThis

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...