Wednesday, October 17, 2012



DKT.  ULIMBOKA KUANIKA WALIOMTESA NA KISHA KUMTELEKEZA.
KIONGOZI WA JUMUIYA YA MADAKTARI DKT.STEVEN  ULIMBOKA.


KIONGOZI wa Jumuiya ya Madaktari Tanzania, Dk Steven Ulimboka,  anatarajiwa kutoa siri  nyeti kuhusu kutekwa na kuteswa kwake na kisha kutelekezwa kwenye  Msitu wa Mabwepande, Bunju, jijini Dar es Salaam.

Vyombo vya habari vimemnukuu, Mmoja wa ndugu ambaye pia ni rafiki i wa karibu wa kiongozi huyo akisema kuwa Dkt Ulimboka , amepanga kuanika hayo katika mkutano wake na waandishi wa habari.ambao huenda ukafanyika katika kipindi cha saa 48.

Alisema Dk Ulimboka, atatumia mkutano huo kueleza siri ya kutekwa kwake.
 “Siku yoyote kuanzia sasa umma, utafahamu ukweli halisi wa kilichompata kijana wetu. Niliongea naye juzi na amenithibitishia kuwa atakutana na waandishi wa habari na kueleza kila kitu katika  masahiba yaliompata,” alisema ndugu huyo

Alisisitiza  “Ni kweli kwamba Steven (Dk. Steven Ulimboka) amepanga kukutana na waandishi wa habari. Anataka kutumia mkutano huo, kuanika wote walioshiriki kumtesa, kumteka na kisha kumtupa katika msitu wa Magwepande,”

Dk Ulimboka alitekwa usiku wa Juni 26 mwaka huu, katika maeneo ya Leaders Club jijini Dar es Salaam na baadaye kusukumizwa kwenye gari, kupigwa, kufungwa mikononi  na miguuni kabla ya kunyofolewa kucha na meno; katika Msitu wa Mabwepande.

DKT. ULIMBOKA AKIWA KATIKA HOSPITALI YA TAIFA YA MUHIMBILI  MARA BAADA YA KUOKOTWA KATIKA MSITU MABWEPANDE
Aliokotwa na wasamaria wema asubuhi yake na kupelekwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili ambako alilazwa kabla ya kupelekwa Afrika Kusini Juni 30 kwa matibabu zaidi.

Tangu aliporejea nchini Agosti 12 mwaka huu, kumekuwa na shinikizo kubwa kutoka ndani na nje ya nchi, kumtaka azungumze kwa madai kuwa kauli yake itasaidia kujulikana kwa ukweli kuhusu kilichompata.

Kufanyika kwa mkutano huo  kunatajwa na wachambuzi wa mambo kuwa kunaweza kuondoa kiwingu hicho, ikiwa ni pamoja na kujibu baadhi ya maswali yaliyobuka juu ya tukio hilo.




No comments:

Post a Comment

AddThis

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...