Serikali imechukua jukumu la kumhudumia msanii na muongozaji wa filamu
Sadick Juma Kilowolo ambaye anatarajia kuondoka wiki ijayo kuelekea India kwa
matibabu.
Katibu wa Shirikisho la Filamu Tanzania (TAFF) Wilson Makubi, alisema
Sajuki ambaye kwa sasa amelazwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili,
amegundulika kuwa ana tatizo la kufeli kwa figo na kwamba yuko chini ya
uangalizi na uchunguzi zaidi.
Alisema kutokana na hali hiyo, serikali imejitolea kumsafirisha msanii
huyo kwa gharama zake na kusaidia katika gharama za matibabu akiwa nchini
India.
“Sajuki anatarajiwa kusafiri wiki ijayo baada ya taratibu zote
kukamilika, hivyo sisi kama TAFF tunathibitisha kuwa hali yake bado
haijatengemaa kama ilivyojulikana hapo awali,” alisema Makubi.
Msanii huyo amekuwa akisumbuliwa na maradhi kwa muda mrefu ambapo mwaka
jana alianza na uvimbe ulioanzia mikononi na baadaye ndani ya mwili kwenye ini
na sehemu tofauti za tumbo.
Msanii huyo alipelekwa India kwa ajili ya kutibiwa, kisha akarejea
nchini baada ya kupata nafuu, ambapo kwa sasa ameugua tena na anahitaji
matibabu ya haraka ikiwamo upasuaji.
No comments:
Post a Comment