TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya
Taifa imejadili na kutolea maamuzi pamoja na mambo mengine suala la
Madiwani wanane waliotangazwa kufukuzwa uanachama na Halmashauri Kuu ya CCM
Mkoa wa Kagera.
Katika maamuzi yake, Kamati Kuu imebatilisha
uamuzi uliofanywa na Halmashauri Kuu CCM ya Mkoa wa Kagera Agosti 13, 2013
wa kuwafukuza
uanachama Madiwani hao.
Hivyo
Madiwani hao wanane ni wanachama halali wa CCM.
Kamati Kuu imetoa uamuzi huo, baada ya
kubaini kuwa Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa wa Kagera haikuzingatia Katiba ya
CCM ya 1977 Toleo la 2012 Ibara ya 93 (15).
Ibara hiyo inasomeka kuwa moja
ya kazi ya Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa ni:-
“Kumwachisha au kumfukuza uongozi
kiongozi yeyote ambaye uteuzi wake wa mwisho unafanywa na Halmashauri Kuu
ya CCM ya Mkoa, isipokuwa kwa suala la kumvua uanachama au uongozi Diwani
lisifanyike hadi Kamati Kuu imearifiwa na kutoa maelekezo”.
Aidha, Kamati Kuu imewaonya Madiwani wa CCM
wa Manispaa ya Bukoba, Mbunge wa Bukoba Mjini na Meya kwa kusababisha
kukosekana kwa utulivu, mshikamano na amani katika Manispaa na Chama.
Kamati Kuu pia imeitaka Serikali kumwagiza
mdhibiti na mkaguzi mkuu wa serikali(CAG) kufanya ukaguzi maalum wa haraka
wa mambo yanayolalamikiwa dhidi ya Meya ili ukweli ujulikane na matokeo ya
uchunguzi huo yasilishwe kwenye baraza la madiwani ili hatua stahiki
zichukuliwe kwa mujibu wa sheria na taratibu zinazoongoza Serikali za
Mitaa.
Wakati tuhuma hizo dhidi ya Meya
zikichunguzwa; Kamati Kuu inawataka Madiwani wa CCM kurejesha
utulivu kwenye Manispaa na Chama kwa ujumla ili kufanikisha utekelezaji wa
Ilani ya Uchaguzi ya CCM na kuwaletea maendeleo wananchi wa Bukoba.
Imetolewa na:-
Nape Moses Nnauye,
KATIBU WA HALMASHAURI KUU YA
TAIFA YA CCM
ITIKADI NA UENEZI
27/08/2013
No comments:
Post a Comment