OBAMA AONGOZA
KURA ZA MAONI UCHAGUZI WA MAREKANI
Kura
za maoni nchini Marekani zinamuonesha Rais Barack Obama akiongoza mbele ya
mshindani wake mkuu, Mitt Romney, huku wakosoaji wakimsakama Romney kwa kauli
zilizowakasirisha wapiga kura juu ya sera ya afya ya Obama.
Hata
kama maoni haya ya wapiga kura wa Marekani yalikusanywa kabla ya kutolewa kwa
video ya siri inayomuonesha Romney
akiwaambia wafadhili wake matajiri kwamba asilimia 47 ya wapiga kura wa
Marekani ni wategemezi wa serikali ambao watampigia kura Obama kuendelea kupata
ruzuku ya serikali na kwamba hajali kuhusu hao, tayari inaonekana kwamba Romney
amekalia kuti kavu.
Rais
Obama ameiita kauli hiyo kuwa ni ya kiongozi asiyewajibika kwa umma.
"Ninapokuwa ninatembelea sehemu mbalimbali kwenye nchi yetu, nakutana na
watu ambao wanajituma sana na ambao wanajali kuhusu nchi hii.
Na matarajio
yangu ni kwamba kama unataka kuwa rais, unalazimika kuwa tayari kufanya kazi
ajili ya kila mtu na sio baadhi yao tu." Amesema Rais Obama.
Hadi
sasa Romney hajaikanusha wala kuomba radhi kwa kauli hiyo, badala yake amesema
kwamba ni maoni yake ambayo yanaonesha tafauti ya kimsingi iliyopo kati yake na
Obama.
Kwa
mujibu wa matokeo ya kura ya maoni yaliyochapishwa leo kwa ushirikiano wa Chuo
Kikuu cha Quinnipiac, gazeti la New York Times na kituo cha televisheni cha CBS
News, Rais Barack Obama anaongoza katika majimbo matatu muhimu ya Virginia,
Wisconsin na Colorado na majimbo mengine yote muhimu yenye wapiga kura
waliokuwa hawajaamua.
Obama
amemtangulia Romney kwa asilimia 51 kwa 45 katika jimbo la Wisconsin, ambako
ndiko nyumbani kwa mgombea mwenza wa Romney, Paul Ryan, wakati katika jimbo la
Virginia akiongoza kwa 50 kati ya 46 za Romney na 48 kwa 47 katika jimbo la
magharibi la Colorado.
Obama
alishinda majimbo yote matatu mwaka 2008, alipokuwa mgombe wa kwanza Democrats
kushinda Virginia tangu mwaka 1964.
Katika
eneo la uchumi, wagombea hao wawili wanachuana vikali katika majimbo yote
matatu, Obama akiongoza kwa asilimia 49 kwa 46 za Romney kwenye jimbo la
Winsconsin, ambapo katika eneo la kimataifa, Obama yuko mbele kwa asilimia 50
dhidi ya 43 za Romney kwenye jimbo la Colorado na 53 dhidi ya 42 kwenye jimbo
la Virginia.
Obama
pia ameongoza kwenye eneo la vita dhidi ya ugaidi, ambapo matokeo yanamuonesha
akiwa na asilimia 50 dhidi ya 41 katika jimbo la Colorado.
Matokeo
haya yalikusanywa kati ya tarehe 11 na 17 Septemba, katika wakati ambapo
maandamano dhidi ya filamu inayoukashifu Uislamu yalipokuwa yamepamba moto
katika sehemu kadhaa duniani, ikiwemo nchini Libya, ambako balozi wa Marekani
na Wamarekani wengine waliuawa mjini Benghazi.
Romney
alikumbana na lawama kali baada ya kumtuhumu Obama kwa kuwaonea huruma
waandamanaji katika kauli aliyoitoa masaa 11 baada ya balozi huyo kuuawa.
Wakosoaji
wake, wakiwamo wa wahafidhina wengi, walimtuhumu Romney kwa kumkashifu rais
kisiasa katika wakati wa mgogoro wa kimataifa kama huo.
No comments:
Post a Comment