Friday, September 14, 2012


waandamanaji  wanaopinga filamu inayomkashifu mtume wao nchini Misri


JE MASHAMULIZI KATIKA BALOZI ZA MAREKANI YANASABABISHWA NA FILAMU?

Mashambulizi katika ubalozi wa Marekani nchini Misri na Libya yaliyotokea jumanne wiki hii yalikuwa ya kutisha, na kifo cha balozi wa Marekani nchini Libya Christopher Steven kinasikitisha 

Mashambulizi haya yanadaiwa kutokana na filamu iliyotengenezwa Marekani ambayo inamdhalilisha Mtume Mohamad. 

Lakini ukweli ni kwamba, sababu ya mashambulizi haya ni kubwa kuliko inavyoonekana, ikionyesha upungufu wa mkakati wa Marekani katika eneo la Mashariki ya Kati, na umuhimu wa nchi hiyo kufikiri upya sera zake kuhusu kanda hiyo. 


Mwaka jana, Libya na Misri zote zilishuhudia mgogoro mkubwa wa kisiasa ambao Marekani ilichukua nafasi kubwa na muhimu. Hata hivyo, Wamisri na Walibya wengi hawaonekani kuwa na shukrani kwa nchi hiyo, na mashambulizi haya mabaya yanaweka wazi hasira walizo nazo. Kwanini? Swali hili lina majibu mengi. 

Kwa muda mrefu Marekani imetaka kuwa na mamlaka katika kanda ya Mashariki ya Kati, na watu katika eneo hilo wamechoshwamitazamo yake katika taifa hilo.

 Miaka iliyopita, Marekani ilianzisha vita dhidi ya ugaidi na kuibadilisha Iraq kuwa nchi yenye machafuko makubwa na kusababisha vifo na majeruhi wengi, huku mamilioni ya watu wakipoteza makazi yao. 

 Marekani imeshindwa kuleta mafanikio katika kanda hiyo, na watu wa eneo hilo wamebaki kwenye dhiki na hali mbaya. Kwa mfano, milipuko na mapigano ya kidini bado vinaendelea nchini Iraq, ukarabati wa nchi unafanyika kwa kasi ndogo, na kuibuka upya kwa kundi la Al-Qaida. 

Mashambulizi haya ni pigo kubwa kwa mpango wa miaka mingi wa Marekani wa kujaribu kuleta muungano wa Mashariki ya Kati kwa kuwaondoa viongozi ambao hawakubaliani nayo, kama vile Iran na Syria. 

Katika hili, Marekani na washirika wake wamekuwa wakilazimisha mabadiliko ya utawala kwa madai ya kuleta demokrasia. Lakini hali katika kanda hiyo bado ni mbaya, na muungano umezidi kuwa dhaifu badala ya kuimarika. 

Sababu nyingine ya hasira za wananchi wa Libya na Misri ni kwamba, upendeleo wa Marekani kwa Israel unasababisha wimbi la chuki katika nchi za kiarabu, hivyo kutikisa msingi wa mkakati wa Marekani katika kanda hiyo. 
 http://www.odt.co.nz/files/story/2012/09/supporters_of_sunni_muslim_salafist_leader_ahmad_a_505232428f.JPG


Zaidi ya hayo, mwenendo wa kisiasa katika nchi nyingi za Mashariki ya Kati umebadilika kufuatia kujitokeza kwa makundi ya kidini, jambo ambalo si zuri kwa Marekani. 

Ucheleweshaji wa Marekani kuanza tena mchakato wa amani wa Mashariki ya Kati pia kumeongeza hasira za wananchi wa kanda hiyo. 

Dunia ilikuwa na matumaini makubwa ya kuendelea kwa mpango wa amani mara rais wa sasa wa Marekani Barack Obama alipochukua madaraka, lakini katika miaka minne iliyopita, serikali ya Obama haijapata maendeleo makubwa katika suala hilo. 

Mwisho, Marekani imedhihirisha kushindwa kusuluhisha suala kubwa la tofauti ya utamaduni. Kufuatia mambo mengi yaliyofanywa na Marekani katika kanda ya Mashariki ya Kati kwa miongo kadhaa, tofauti ya kitamaduni kati ya Marekani na kanda hiyo imezidi kuwa kubwa. 

Waandamanaji wakiushambulia ubalozi wa Marekani  nchini Yemen

 Kwa kuzingatia yote haya, ni wazi kuwa mashambulizi katika ubalozi wa Marekani nchini Misri na Libya zinapaswa kuikumbusha Marekani kuwa, wakati umefika wa kufikiria upya sera zake kuhusu Mashariki ya Kati, ama sivyo, itashindwa kutimiza lengo lake katika kanda hiyo.

No comments:

Post a Comment

AddThis

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...