Friday, April 6, 2012

Rais Mutharika afariki dunia

 

 

Mwanzoni redio ya taifa ilikuwa imetangaza kwamba Mutharika, mwenye miaka 78, angelipelekwa Afrika Kusini kwa matibbabu zaidi, lakini inaonekana kwamba alishafariki dunia wakati alipofikishwa hospitali.


Kwa mujibu wa katiba ya nchi hiyo, Makamu wa Rais Joyce Banda, ndiye anayechukuwa nafasi ya kiongozi wa nchi, ingawa kuondolewa kwa Banda kutoka chama tawala hapo mwaka 2010 kunaweza kutatiza kipindi cha mpito.

Mutharika, aliyewahi kufanya kazi kama mchumi kwenye Benki ya Dunia, amekuwa akituhumiwa kwa kushindwa kuongoza na kutokuuendeleza uchumi wa nchi hiyo. Inasemekana alikuwa akimtayarisha mdogo wake, Waziri wa Mambo ya Nje Peter wa Mutharika, kuwa mrithi wake. Mara kadhaa, Peter amekuwa akionekana akikaimu wadhifa wa kaka yake anapokuwa hayupo.


Maandamano ya mwaka 2011 dhidi ya Mutharika mjini Lilongwe. Maandamano ya mwaka 2011 dhidi ya Mutharika mjini Lilongwe.

Polisi katika mji mkuu, Lilongwe wameimarisha usalama, tangu tangazo la maradhi ya ghafla ya Mutharika ilipotangazwa hapo jana, huku wanajeshi wakionekana karibu na nyumba ya Banda.

Kabla ya kifo chake, hali yake ilionesha kupata huruma za watu katika mji wa Blantyre, mji mkuu wa kibiashara wa Malawi, ambako wengi wanamuona kiongozi huyo kama sababu ya upungufu mkubwa wa mafuta, chakula na fedha za kigeni.

Baada ya kupokea taarifa ya kifo hicho, dereva mmoja wa teksi mjini humo akiwa kwenye msongo wa kusubiri mafuta, aliliambia Shirika la Habari la Reuters kuwa "huenda mwisho wa mateso uko karibu."

Baada ya Mutharika kuchukuwa madaraka ya urais hapo mwaka 2004, uchumi wa Malawi uliimarika sana. Lakini licha ya uimarikaji huo uliochukua miaka saba mfululizo, mabishano ya kidiplomasia na mfadhili mkubwa wa Malawi, Uingereza, yalichangia kuirudisha nyuma nchi hiyo ya kusini mwa Afrika.


Rais Bingu wa Mutharika Malawi katika jukwaa la uchumi duniani. Rais Bingu wa Mutharika Malawi katika jukwaa la uchumi duniani.

Ukatwaji wa misaada ulipelekea kupungua kwa uingizwaji wa mafuta, chakula na madawa na kuporomoka kwa sarafu ya Kwacha ya nchi hiyo. Maandamano dhidi ya utawala wa Mutharika hapo mwaka jana yalikabiliana na ukandamizaji mkali wa polisi na kumalizika kwa vifo vya waandamanaji 20.

Waandamanaji walikuwa wanapinga kudorora kwa uchumi na pia tabia ya udikteta ambayo Mutharika alishukiwa kuanza kuwa nayo. Kupoteza kwake umaarufu nje ya nchi yake, kulikwenda sambamba na ugomvi baina yake na viongozi wenzake serikali, ukiwemo ule wa Makamo wa Rais, Joyce Banda, ambaye mwaka jana alimfukuza kwenye chama tawala, lakini akabakia na nafasi yake ya umakamo rais.

Uchaguzi mwengine ulikuwa unapangwa kufanyika nchini Malawi mwaka 2014.


Angola yatimiza muongo mmoja wa amani

 Kulingana na Benki Kuu ya Dunia, uchumi wa taifa hilo la Kusini mwa Afrika lenye watu zaidi ya milioni 20, umeongezeka kwa asilimia 12, likishika namba ya pili barani humo kwa usafirishaji wa mafuta baada ya Nigeria.
Hayo yakitazamwa kama mafanikio makubwa kwa taifa la Angola, kukiwa na mafanikio ya ujenzi wa miundo mbinu kama vile barabara, viwanja vya ndege na mikakati ya ujenzi wa makazi mapya kwa baadhi ya maeneo ya nchi hiyo.

Lakini kwa upande mwingine, malalamiko yapo kwa utawala wa Rais Jose Eduard dos Santos kuwa amejilimbikizia mamlaka na kuwafanya wananchi wengi kuendelea kuwa masikini mno.


Vijana wengi wanasadikiwa kukosa ajira, jambo ambalo limewafanya mara kadhaa kuingia barabarani kuandamana dhidi ya utawala.


Mkuu wa Majeshi Angola, Jenerali Armando da Cruz Neto (kushoto) na mkuu wa Majeshi wa UNITA, Abreu Muengo Ukwachitembo "Kamorteiro", wakibadilishana hati za mkataba wa amani. Mkuu wa Majeshi Angola, Jenerali Armando da Cruz Neto (kushoto) na mkuu wa Majeshi wa UNITA, Abreu Muengo Ukwachitembo "Kamorteiro", wakibadilishana hati za mkataba wa amani.

Vijana hao wakianza kufanya harakati kama zile za mataifa ya Kiarabu kuanza kufanya maandamano na kusisitiza kudai haki zaidi kutoka kwa utawala huo wa Angola pakiwa na miito mingi ya kufanya hivyo kwenye mitandao ya intaneti.

Marcolino Moco, ambaye aliwahi kuwa Waziri Mkuu wa taifa hilo, ni miongoni mwa watu wanaoulalamikia utawala huu wa Rais Dos Santos akisema bayana kuwa sasa utawala wa Angola unatakiwa kutazama kwa kina hali ya siasa ulimwenguni ilivyo kama yale yanayotokea katika mataifa ya Kaskazini mwa Afrika huku uchaguzi wa Bunge ukipangwa kufanyika Septemba mwaka huu. Rais Dos Santos mwenye miaka 69 sasa, amekuwa kiongozi wa taifa hilo tangu mwaka1979.

Elias Isaac anaungana na kauli ya Waziri Mkuu Msaafu Moco kwa kusema kuwa serikali ya Angola haina uwazi katika mambo yake akituhumu kwa kupotea zaidi ya dola bilioni 32 fedha za umma na pia kushindwa hata kuhifadhi vizuri kumbukumbu hizo.

Hali ya maisha kwa Waangola wengi inaonekana bado ni duni mno kwani watu milioni 16.5, kati ya milioni 20 wa taifa, hili wanaishi chini ya dola mbili kwa siku. Umoja wa Mataifa ukiliweka kuwa taifa la148 kati yamataifa 187 katika maendeleo.

Angola ilijipatia uhuru wake kutoka Ureno mwaka1975, lakini mara baada ya uhuru huo iliingia katika vita vya wenyewe kwa wenye mpaka mwaka 2002 ambapo mshindi wa vita hivyo alikuwa Rais wa sasa Dos Santos chini ya chama cha Kikomunist cha MPLA, akikishinda chama cha UNITA. Vita hivyo viligharimu maisha ya watu zaidi ya nusu milioni na kudumu kwa miaka 27.

No comments:

Post a Comment

AddThis

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...